Mabasi ya Mwendokasi kuwa na intaneti na viyoyozi (AC)

0
30

Serikali imesema kuwa ina mpango wa kuweka huduma ya intaneti (Wi-Fi) na viyoyozi katika mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) kwa lengo la kukuza ushindani na kutoa huduma za kisasa.

Ameyasema hayo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Charles Msonde hapo jana wakati akifungua kikao kilichowakutanisha wadau wa usafiri ardhini nchini, kwa lengo la kujadili nauli mpya za mabasi yaendayo haraka.

Dk. Msonde amesema, Serikali kupitia DART imeandaa mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za usafiri kwa watumiaji wa makundi tofauti tofauti ikiwemo kuboresha huduma za usafiri kwa wanafunzi, watu wenye mahitaji maalumu na kina mama.

DART yapendekeza nauli kuwa TZS 1,500

“Nimefahamishwa kuwa DART ina malengo ya kufanya maboresho makubwa katika kipindi cha muda mfupi ili kukuza ushindani na utoaji wa huduma za kisasa. DART inakwenda kuanzisha mabasi yenye viyoyozi pia kuanza kutumia mfumo wa TEHAMA katika ukusanyaji wa nauli na upatikanaji wa intaneti katika mabasi yetu,” amesema.

Mbali na hayo, amesema maoni ya wadau wa usafiri ni muhimu katika upangaji wa nauli mpya za mabasi yaendayo haraka, na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inaendelea kupokea maoni ndani ya siku saba.

Send this to a friend