Mambo 5 unayofanya kila siku yanayopunguza muda wako wa kuishi

1
34

Kila mtu anatamani kuishi muda mrefu, wengi wanajua nini cha kufanya au kutokufanya ili kufikia lengo hilo, lakini sio wote wenye utayari wa kufanya mambo hayo kwa sababu huambatana na kujinyima baadhi ya vitu.

Kwa mujibu wa watafiti mbalimbali duniani, mambo tunayofanya au vyakula tunavyokula kila mara yanaweza kutengeneza madhara ya muda mrefu kwenye maisha yako na kupunguza au kuongeza muda wako wa kuishi.

Tukiangazia zaidi mada hiyo, tovuti ya afya ya Verywell Health imeanisha mambo kadhaa ambayo ukifanikiwa kuyaacha utajiweka katika nafasi ya kuishi kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na yule anayefanya mambo hayo.

Haya ni baadhi tu ya mambo ya kuepuka ili kuongeza muda wako wa kuishi;

Vyakula vilivyosindikwa
Kile unachokula sasa kinaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha yako kwa muda mrefu. Unashauriwa kula vyakula vinavyojumuisha matunda, mboga mboga na vyakula vya nyuzinyuzi kwa kuwa ni kinga ya magonjwa ya moyo, kisukari, unene uliokithiri, shinikizo la damu na hata saratani.

Uvutaji wa Sigara
Taasisi za kitaifa za afya (NIH) inasema utumiaji wa tumbaku unasalia kuwa sababu inayozuilika ya kifo. Baadhi ya makadirio yanaonesha kuwa kuvuta sigara kunaweza kukupokonya miaka 10 ya kuishi. Kumbuka kwamba wanafamilia wako pia watafaidika kutokana na kukaa kwako bila tumbaku kwa sababu hawataathiriwa tena na moshi hatari wa sigara.

Kukaa peke yako
Kukaa na watu wengine kunaweza kuwa kichocheo kizuri cha maisha marefu, haswa kwa kukusaidia kudhibiti mfadhaiko na kuimarisha mfumo wako wa kinga. Mahusiano mazuri hukuweka imara, wakati mahusiano mabaya yanaweza kukuacha katika hali mbaya ya akili na kukuweka katika hatari ya shambulizi la moyo.

Kukesha usiku
Kiwango cha usingizi unachopata kinaweza kuathiri muda wako wa maisha. Kulala kidogo sana (chini ya saa sita) au kwa kiasi kikubwa zaidi (zaidi ya saa tisa) huwaweka watu katika hatari kubwa ya kifo. Usingizi mzuri wa usiku unaweza kukusaidia kuzuia mfadhaiko, mshtuko wa moyo, na ugonjwa wa moyo.

Acha kukaa siku nzima
Mazoezi yametajwa kupunguza hatari yako ya kupata magonjwa yanayohusiana na umri kama vile ugonjwa wa moyo na mishipa, kisukari, kiharusi, na baadhi ya saratani, huku ukiimarisha mifupa na misuli yako na kuongeza muda wako wa kuishi kwa ujumla.

Utafiti wa mwaka 2011 uligundua kuwa dakika 15 za mazoezi ya nguvu ya wastani kila siku zitakusaidia kuishi miaka mitatu ya ziada. Utafiti pia umeonesha kuwa mazoezi yanaweza kupunguza kuzeeka kwenye kiwango cha seli.

Zingatia haya na mengine kujiweka katika hali ya nzuri ya kiafya wakati wote.

Send this to a friend