Hatma ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imepangwa kujulikana leo ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha itakwenda kuamua iwapo kiongozi huyo wa zamani ataachiliwa huru ama atakwenda kutumikia kifungo.
Sabaya alikamatwa Mei 27, mwaka jana wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa na wenzake sita walifikishwa mahakamani Juni 4, 2021 kwa makosa matano ya uhujumu uchumi likiwemo la kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, kujihusisha na vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha.
Waziri Bashungwa ampa RC Makalla siku saba
Aidha, katika kesi ya uhujumu uchumi inayotarajiwa kutolewa hukumu leo, mbali na Sabaya inawajumuisha watuhumiwa wengine ambao Enock Mnkeni (41) Watson Mwahomange (27), John Aweyo, Sylvester Nyegu (26), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).
Awali, katika makosa matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Sabaya na wenzake wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na baadaye hukumu hiyo ilitenguliwa Mei 6, 2022 baada ya kubaini dosari zilizojitokeza katika mwenendo wa kesi ya msingi katika mahakama ya chini na kubakiwa na kesi moja ya kutolewa hukumu.
Machi 31 mwaka huu Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza shauri hilo la jinai, alisema atatoa hukumu hiyo leo baada ya pande zote kuwasilisha hoja zao za majumuisho.