Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amesema hana mpango wa kugombea urais wa Tanzania mwaka 2025, badala yake anamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kugombea nafasi hiyo.
Membe ambaye pia alikuwa mgombea wa nafasi ya Urais 2020, kupitia Chama cha ACT Wazalendo ameyasema hayo baada ya kurudi katika Chama cha Mapinduzi hivi karibuni.
“Mwaka 2025 ni mama huyu. Natoa msimamo mapema kabisa na ninasema kutoka kwenye dhamira ya moyo wangu. Taifa limezaa viongozi sita, watano wanaume, mwanamke mmoja. Dunia ingetushangaa na itatushangaa sana tukianza kumtenga na kumsimanga,” amesema Membe.
Hata hivyo ameongeza kuwa “mama amejitahidi kadri ya uwezo wake, ni lazima tumpe nafasi yake ya kugombea tena 2025. Mimi nimesema wazi, na nimerudi Chama cha Mapinduzi, nitamuunga mkono,” ameongeza.
Membe alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kuanzia mwaka 2007 hadi 2015. Pia amekuwa Mbunge wa jimbo la Mtama kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.