Dkt. Shita Samwel amewashauri wasichana kuacha matumizi ya vidonge vya majira (Oral Contraceptive pills) pamoja na vidonge vya dharura vinavyojulikana kama Emergency contraceptive pills (EPCs) kiholela bila kupata ushauri wa kitaalamu.
Kwa mijibu wa daktari, baadhi ya wasichana kuanzia umri wa miaka 12 hadi 18 wamekuwa wakitumia dawa hizo bila kujua kuwa zinaweza kuleta madhara ikiwa mtumiaji hakupata ushauri kutoka kwa daktari.
Baadhi ya madhara yanayoweza kujitokeza mara kwa mara kwa watumiaji holela ni pamoja na kuumwa kichwa na hata kupata kipanda uso (migraine), kutoka chunusi, kupata vipele na muwasho wa mwili.
Pia, matiti kuuma na kuvimba, kupata uvimbe mgumu mfano wa kitenesi (cysts), baadhi hupata saratani ikiwamo ya ini kwa walioanza kutumia katika umri mdogo, kichefuchefu au kutapika, uoni hafifu na damu kuvilia machoni.
Madhara ya kiafya ya kuchangia ‘helmet’
Madhara mengine ni kuyumba kwa mzunguko wa hedhi na kutokwa na mabonge ya damu wakati wa hedhi, hali inayowatokea baadhi ya vijana, kupungua kwa mihemko ya hamu ya kujamiiana, mabadiliko ya hisia, kinga kuwa dhaifu hivyo kupata maambukizi ya mara kwa mara ikiwemo ukeni na nyumba ya uzazi na kupata unene.
Kuvimba miguu na maumivu katika ugoko, kupata tatizo la umanjano (jaundice), mkojo kubadilika rangi, maumivu katika tumbo upande wa kulia chini ya mbavu.
Daktari ametoa ufafanuzi kwa wale ambao tayari wana magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu na wanatumia vidonge hivyo, wapo katika hatari ya kupata kiharusi (stroke).
Aidha, amesisitiza kuwa madhara hayo huwapata mara nyingi wasichana, lakini pia umuhimu wa vidonge hivyo ni mkubwa kuliko madhara hivyo wasichana waepuke kutumia vidonge hivyo kiholela bila kupata ushauri wa daktari.