Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imewaagiza wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo yote ya mikusanyiko ya watu ikiwemo maeneo ya masoko kutenga maeneo maalumu ya kuvuta sigara na tumbaku.
Meneja wa TMDA wa Kanda hiyo, Anitha Mshighati ameyasema hayo wakati akieleza mkakati wa mamlaka hiyo wa kuelimisha wananchi juu ya matumizi ya tumbaku na sigara.
Aidha, ameongeza kuwa mamlaka inakusudia kufanya uchunguzi kubaini aina ya madawa ya kulevya ama vilevi vinavyodaiwa kuchanganywa kwenye shisha baada ya kuonekana wavutaji wengi wa bidhaa hiyo wanalewa haraka ukilinganisha na asili ya bidhaa hiyo.
Ameongeza kuwa, mamlaka inakuja na mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za matumizi ya sigara pamoja na kusisitiza uvutaji wa kistaarabu ili kuondoa kero kwa watu wengine.
Hata hivyo, amesema baada ya elimu kutolewa kwa wananchi watafanya ukaguzi wa utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watakaokaidi maagizo hayo.