Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ametoa onyo kwa mbunge wa jimbo laTarime Vijijini, Mwita Waitara kwa kudharau maamuzi ya Spika kuielekeza Serikali kufanya uchunguzi juu ya madai ya mauaji kwa wakazi wa Tarime.
Kwa mujibu wa Spika, baada ya kuipa Serikali siku 90 ya kufanya uchunguzi juu ya malalamiko yaliyotolewa na mbunge huyo, alikwenda kutoa malalamiko katika vyombo vya habari akidai kuwa Serikali haiwezi kujichunguza yenyewe kwakuwa ndiyo inayolalamikiwa.
Spika amenukuu malalamiko ya mbunge huyo yaliyochapishwa katika gazeti la Raia Mwema, toleo namba 1031 la Juni 10 mwaka huu.
“Ni vigumu Serikali inayotuhumiwa kutenda jambo fulani kwenda kujichunguza, badala yake Bunge lilipaswa kuunda kamati teule kuchunguza na taarifa kuwasilishwa kwake si kama alivyofanya Spika.”
Ameendelea kunukuu “Hifadhi ya Serengeti ni ya Serikali, sasa Serikali inawezaje kujichunguza kwa kuwa Serikali inalalamikiwa? na Spika amewahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilitakiwa iundwe kamati teule ya bunge ikachunguze kisha taarifa iwasilishwe bungeni.’
Baada ya kuyasoma malalamiko hayo bungeni, amesema jambo alilolifanya mbunge Waitara linaenda kinyume na kanuni na taratibu za uendeshaji bunge ambazo zinaweka wazi ni nini mbunge anapaswa kufanya endapo hajaridhishwa na maamuzi ya Spika.
Hata hivyo, Spika ameongeza kuwa kwa kitendo alichokifanya Waitara ni kupuuza maamuzi ya Spika aliyoyatoa, kuvunja heshima na kushusha hadhi ya Spika pamoja na kudhalilisha kwa makusudi mwenendo wa shughuli za bunge hivyo Spika ametoa onyo kwa mbunge huyo na kumtaka asirudie tena.