Mambo yanayokuweka kwenye hatari ya kuugua ugonjwa wa Ini

0
15

Virusi vya homa ya ini vipo vya aina 5 (A,B,C,D,E).
Aina mbili za virusi (B Na C ) zimetajwa kuwa ndio sababu kuu za ugonjwa wa homa ya ini ambayo husambaa kupitia damu na majimaji ya mwili.
Wataalamu wa afya wanasema virusi hivi vina uwezo wa kusambaa na kuambukiza mtu mara 100 zaidi ya Virusi vya UKIMWI.
Njia za maambukizi ya ugonjwa wa Ini
• Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Mama aliye na maambukizi anaweza kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua, iwapo hakuna juhudi za tiba za kuzuia maambukizi, kuna uwezekano hadi asilimia 90 kwa mama kumuambukiza mtoto.

• Kufanya mapenzi na mtu mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini
• Kuchangia vifaa vyenye ncha kali kama sindano hasa kwa watumiaji wa madawa ya kulevya au wachora ‘tattoo’, miswaki etc
• kuongezewa damu ambayo ina maambukizi ya homa ya ini
Nani yuko katika hatari ya kuambukizwa
• Watoto wachanga waliozaliwa na mama aliye na maambukizi ya virusi vya homa ya ini
• Watu wanaofanya biashara ya ngono
• Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao
• Watu wanaojidunga dawa za kulevya
• Mtu mwenye mpenzi ambaye anaishi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini
• Wafanyakazi wa Sekta ya afya
• Watu wa familia wenye ndugu anayeishi na maambukizi ya kudumu ya Virusi vya homa ya ini
• Wagonjwa wa figo wanaotumia huduma za kusafisha damu (Dialysis)

Jinsi ya kujilinda
Dhibiti matumizi yako ya dawa
Tumia dawa ulizoandikiwa na mtaalamu wa afya, au daktari wa eneo lako. Usitumie dawa ulizoandikiwa pamoja na pombe au dawa za kulevya. Dawa zingine zikitumiwa kwa kipimo cha juu zinaweza kuwa sumu kwenye ini lako (kama vile paracetamol).

Punguza au acha kunywa pombe
Kadri unavyopunguza unywaji wa pombe, ndivyo unapunguza hatari ya kupata madhara yanayotokana na pombe ikiwemo magonjwa ya ini.

Acha kuvuta sigara, bangi au dawa zingine za kulevya
Sumu na kemikali zilizomo kwenye sigara zinaweza kudhuru ini lako. Matumizi ya kipimo cha juu cha bangi yanaweza kuongeza uharibifu wa ini. Kuna hatari ya kupata kansa ya ini ikiwa unatumia sigara au bangi.

Tumia mbinu salama ya kujidunga
Tumia kifaa safi na chako mwenyewe cha kujidunga, kuwa makini na kujichora chale au kujidunga mwilini. Chagua kituo ambacho kinafuata njia salama za uzuiaji wa maambukizi, kamwe usishiriki kifaa cha kujidunga na mtu mwingine.
Shiriki ngono salama
Tumia kondomu wakati wa kushiriki ngono. Hatua hii itakulinda dhidi ya kupata maambukizi ya virusi kupitia majimaji ya ngono au damu.