Tanzania mwenyeji tuzo za MTV Africa Music Award 2023

0
16

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais na Meneja Mkuu wa Paramount Africa and Peer Lead BET International, Monde Twala, ambapo wamekubaliana kushirikiana katika kuiwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa tuzo za MAMA- MTV Africa Music Award kwa mwaka 2023.

Mchengerwa amekutana na Monde Twala Jijini Los Angeles nchini Marekani wakati wa hafla ya utoaji tuzo za BET kwa mwaka 2022, lililofanyika June 26 na amemwelezea nia na sababu ya Tanzania kutaka kuwa mwenyeji wa tamasha hilo kuwa, ni kuongeza ushawishi kwa vijana wa kuendelea kufanya vizuri katika sekta za burudani pamoja na kuitangaza zaidi Tanzania.

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zimekubaliana kuungana kwenye kutafuta washirika katika kuendesha tuzo hizo, na kuridhia kuwa maandalizi yaanze mara moja, huku wakipendekeza muda wa tamasha hilo la utoaji tuzo kufanyika Oktoba 2023 jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Tawala amesema anaiona Tanzania kama eneo lenye vipaji vya hali ya juu katika sekta ya Sanaa, na burudani ambavyo havijaonekana na kutumika kwa manufaa ya nchi na manufaa ya wasanii wenyewe, na kuahidi kushiriki moja kwa moja katika kuwezesha kufanyika kwa tuzo hizo nchini Tanzania kwa mwaka 2023.

Viongozi hao pia wanatarajia kutembelea kampuni mbalimbali za uzalishaji wa filamu na muziki, lengo likiwa ni kutengeneza mahusiano na kuona namna Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inavyoweza kuwawezesha wataalamu kutoka katika makapuni hayo maarufu duniani kuwajengea uwezo wazalishaji wa muziki na filamu wa hapa nchini Tanzania.

Send this to a friend