Wajawazito watozwa gharama tofauti za kujifungua kulingana na jinsia ya mtoto

0
25

Wananchi wa Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo wilayani Iramba mkoani Singida wamelalamikia gharama za wajawazito wanapokwenda kujifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi kutozwa TZS 60,000 pindi anapozaliwa mtoto wa kiume na TZS 50,000 kwa mtoto wa kike na kujifungua kwa operesheni wanatozwa kati ya TZS 200,000 hadi 300,000.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Bilinith Mahenge wakati akizungumza na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara katika mfululizo wa ziara ya kusikiliza kero.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunatozwa fedha nyingi tunapokwenda kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Kiomboi, mfano anapozaliwa mtoto wa kiume tunatozwa Shilingi 60,000, mtoto wa kike Shilingi 50,000 na operesheni 200,000 hadi 300,000 tunaomba utusaidie kwa hili.” amedai mmoja wa wananchi.

Dk. Mahenge amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kufuatilia suala hilo na waangalie huduma za mama kujifungua zinavyotolewa na kama wanatoa stakabadhi.

“DC fuatilia suala hili mjue kama wapo watu wanakiuka taratibu basi hatua zichukuliwe haraka,” amesema.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Hyasinta Alute amemuahidi Mkuu wa Mkoa kufuatilia suala hilo na kujua mama huyo alitozwa fedha hizo katika kituo gani ili kuchua hatua.

Send this to a friend