Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imesema inafanyia utafiti dawa za nguvu za kiume aina ya Viagra pamoja na kuwekea mkakati dawa zinazotumika kuzuia mimba aina ya P2 kwa lengo la kudhibiti uholela wa utumiaji wake.
Ameyasema hayo Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika maonyesho ya Kimataifa ya biashara maarufu Sabasaba.
Fimbo amesema utumiaji holela wa dawa za jamii ya kuzuia mimba na za kuongeza nguvu za kiume zimekuwa zikitumika ndiyo sivyo na hivyo kuwaletea madhara watumiaji.
“Tumekuwa tukipata ripoti mbalimbali, watu wamekuwa wanapoteza maisha, wito wetu mkubwa mtu akitaka kutumia hizi dawa ni vyema apate ushauri kwa mtaalamu wa afya,” amesema Fimbo.
Wajua, si kosa trafiki anapokuomba leseni hapo hapo ukawa huna
Aidha, ametoa tahadhari katika upande wa matumizi ya dawa za P2 ambazo zimekua zikitumiwa na watoto wa shule na wanawake kwa ajili ya kuzuia mimba ambazo zimekuwa zikileta madhara makubwa na hata vifo.
“Tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunatoa elimu kwa watoto wetu wa kike na wanawake kuacha kutumia dawa hizi kiholela kwa sababu zinasababisha vifo visivyotarajiwa na kuelimisha jamii matumizi sahihi ya kutumia,” amesisitiza.