Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini [RUWASA] una mpango wa kufunga mita za maji 350 kwenye mikoa 25 nchini isipokuwa Dar es Salaam kwa lengo la kufanya majaribio ya kulipa ankara za maji kabla ya matumizi.
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Clement Kivegalo amesema lengo la kufunga mita za kulipia kabla ni kuhakikisha wanakusanya fedha ipasavyo kutokana na matumizi ya maji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA, Prof. Idrissa Mshoro amesema ufungaji wa mita hizo unaenda sambamba na matumizi ya bei kikomo za maji nchini ambazo zimefanyiwa utafiti wa kutosha.
“Bei za maji kikomo zitaanza kutumika Agosti Mosi, mwaka huu na zitatumika katika kipindi cha mwaka mmoja na baada ya hapo zitafanyiwa marekebisho,” amesema.
Ujenzi Daraja la JP Magufuli (Kigongo – Busisi) wafikia 47.3%
Amesema katika bei kikomo, kaya moja kwa mwezi itatakiwa kulipa ankara ya maji shilingi 15,000 kama maji hayo yanasukumwa na jenereta inayotumia dizeli, na kwa maji ya pampu ya mkono au maji ya mserereko italipa TZS 5,000.
“Kaya italipa 7,000 kwa mwezi kama maji yanasukumwa kwa umeme wa jua, na shilingi 10,000 kama maji yanasukumwa na umeme wa TANESCO,” amesema.
Katika hatua za awali za majaribio, miongoni mwa maeneo yatakayofungwa mita hizo ni Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga.