Mkurugenzi mpya TPA apewa siku 14 Bandari ya Bagamoyo
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete ametoa siku 14, kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbosa kuwasilisha ripoti ya vitu vyote muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Bagamoyo.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa bandari hiyo mkoani Pwani, Mwakibete amesema kuboreshwa kwa bandari hiyo kutarahisha shughuli za utalii nchini na hivyo kukuza pato la wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
“Kwa kuwa eneo hili la Bagamoyo ni muhimu sana kwa utalii, nampa Mkurugenzi Mkuu wa TPA wiki mbili alete watalaam hapa waangalie vitu muhimu vya kuboresha,” amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Aidha, amesema pamoja na maboresho ambayo Serikali imejipanga kuyafanya kwa bandari, bado inaendelea na mkakati wake wa kurasimisha bandari bubu zinazozunguka eneo la Bahari ya Hindi ili kuweza kupunguza biashara za magendo ambazo zimekuwa zikiendelea kufanyika bila usimamizi mzuri.