Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema jumla ya Watanzania milioni 2.08 hawajakamilisha dozi ya pili ya UVIKO-19, hivyo kuwataka kurudi kwenye vituo vya afya ili kukamilisha kinga inayoshauriwa.
Ameyasema hayo baada ya kikao cha pamoja na Mratibu mkuu wa kimataifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19, Dk Ted Chaiban pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango na Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Kuna watu zaidi ya milioni 2 hawajarudi kwenye dozi ya pili ya chanjo ya UVIKO-19, kwa hiyo nihimize warudi kupata dozi ya pili ili kupata kinga kamili dhidi ya ugonjwa huu wa Covid-19,” amehimiza Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa, viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) vinaeleza ili kupata kinga ya jamii angalau asilimia 70 ya watu wote wanatakiwa kuchanjwa.
Waziri Ummy amesema hadi kufikia Julai 6, 2022 watu milioni 8.5 sawa na asilimia 27 walikuwa wamechanjwa, huku upande wa maambukizi akieleza kuwa wagonjwa wameongezeka mpaka kufikia 14 kutoka wagonjwa watano Juni 5 mwaka huu.