Maelekezo 7 ya Dkt. Mpango katika kukuza Kiswahili duniani

0
13

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa maelekezo saba ili kukuza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili nchini na ulimwenguni, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es salaam.

1. Wizara na Taasisi za Serikali ziendelee kutekeleza maagizo ya Serikali yaliyokwisha kutolewa kwamba;
– Nyaraka za mawasiliano za wizara na idara zake ziwe kwa lugha ya Kiswahili. Na kwamba mikutano, warsha, semina, mijadala ya umma ziendeshwe kwa lugha ya kiswahili.

– Majina ya barabara, mitaa, mabango, fomu za usaili na maelekezo ya matumizi ya dawa zote, bidhaa na huduma zikandikwe kwa Kiswahili.

2. Taarifa za miradi na mikataba inayohusu wananchi ni lazima ziwe kwa lugha ya Kiswahili. Lengo ni kuwawezesha wananchi kuelewa kila jambo muhimu katika ustawi wa maisha yao.

3. Sheria na kanuni ambazo bado hazijatafsiriwa, zitafsiriwe na wizara na taasisi zinazosimamia sheria na kanuni hizo kwa kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili, wataalam wengine wa Kiswahili na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

4. Vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili vihakikishe vinatumia Kiswahili fasaha na sanifu, huku vikizingatia kwa dhati sarufi ya Kiswahili. Pale anaposhirikishwa mtu anayeongea lugha isiyo ya Kiswahili, chombo cha habari kinachohusika kitoe tafsiri ya maneno yasiyo ya Kiswahili ili wananchi waelewe kinachozungumzwa.

5. Agizo lililokwisha tolewa kwa balozi zote za Tanzania, kuanzisha vituo vya kufundisha lugha ya Kiswahili. Balozi zote ziwatumie wataalam wa lugha za Kiswahili waliosajiliwa kwenye kanzidata ya BAKITA na BAKIZA.

6. BAKITA kwa kushirikiana na BAKIZA, ziendelee kuwa wabunifu katika kuzalisha misamiati ya Kiswahili ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.

7. Wizara na taasisi husika wahakikishe mfumo wa kufundisha Kiswahili kwa wageni kwa njia ya mtandao ‘Swahili Pride’ unatumika kikamilifu.

Send this to a friend