Utafiti uliofanywa na Serikali umeonesha kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimepungua kutoka asilimia 10.3 mwaka 2014 hadi asilimia 9.0 mwaka 2021, huku vijana milioni 12.5 sawa na asilimia 87.8 ya nguvu kazi ya vijana nchini wakiwa wameajiriwa au kujiajiri.
Katika mwaka 2021/2022, Serikali imesema imechukua hatua za makusudi hususani utekelezaji wa miradi ya kielelezo, ujenzi wa viwanda, sambamba na kuimarisha sekta binafsi kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha bungeni mapitio ya mwelekeo wa kazi za serikali na matumizi ya fedha katika ofisi yake alieleza kuwa vijana 22,899 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Alisema kati ya hao, vijana 14,440 wakiwemo vijana wenye ulemavu 349 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi katika fani za ufundi stadi, katika vyuo na taasisi 72 nchini.
Aidha, Sekta ya kilimo imeendelea kuongoza kwa kutoa zaidi ya asilimia 63 ya ajira kwa vijana, huku idadi ya jumla ya ajira (kujiajiri na kuajiriwa) zilizozalishwa nchini kuwa ni 584,333.