Halamshauri ya jiji la Dar es Salaam ipo katika hatua za kutunga sheria ndogo ya kuwashughulikia ombaomba ikiwemo kuwashitaki watu wote wanaowapatia fedha.
Watu waliotajwa kuathirika zaidi ni watoto ambao hutumiwa kuomba fedha huku wasimamizi wao wakiwa wamekaa kivulini, hali inayochangia ukatili na wengi kuishia mitaani bila kwenda shule.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Makwiro kwa niaba ya makatibu tawala wote wa mkoa wa Dar es Salaam, na kwamba Manispaa ya Kinondoni na Ilala ndiyo waathirika wakubwa wa suala hilo kwa kuwa kila wanapoondolewa hukimbilia manispaa nyingine.
“Ombaomba wapo kwa sababu kuna watu wana hela kutupita hata sisi, wakimaliza kuomba mchana, jioni wanaoga vizuri sasa sisi kama jiji la Dar es Salaam tumeenda mbali zaidi na sasa tunaandaa sheria ndogondogo ili kuwakamata sambamba na wale wanaotoa fedha kuwapa ombaomba,“ amesema.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Alex Mtaboneka amesema juhudi za kukomesha ukatili dhidi ya watoto lazima ziendane na kuwaangalia pia waganga wa tiba asili kwa kuwa sasa wanaelekea kurasimishwa kwa kuitwa waganga wa tiba asili.