Mifugo 314 yakamatwa kwa kuingizwa nchini kinyume na taratibu

0
15

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU) Tanzania, Simon Pasua amesema Julai 24 mwaka huu Jeshi la Polisi lilikamata mifugo takribani 314 katika kijiji cha Ngoyani tarafa ya Megwe wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro ambayo imeingizwa nchini bila kufuata utaratibu.

Amebainisha kuwa, uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa mifugo hiyo imeingizwa nchini ikitokea nchi jirani kwa ajili ya kutafuta malisho, hivyo taratibu za kisheria zinaendelea kuchukuliwa kuhusu mifugo hiyo.

Aidha, amesema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo na kulisha katika mashamba ya wakulima bila kujali kuwa mashamba hayo yana mazao na kufanya uharibifu mkubwa, hali inayopelekea migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

Kamanda Pasua ametoa onyo kwa wafugaji wote nchini wenye tabia ya kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima ambapo amesema waache mara moja tabia hiyo na kufuata maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Send this to a friend