Makamba: Tanzania kuuza umeme Afrika ifikapo 2025

0
26

Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kilovolti 400 kutoka Iringa, Tanzania hadi Zambia (TAZA) utaanza kutekelezwa Januari mwakani na kukamilika Januari 2025 kwa gharama ya TZS trilioni 1.4

Mradi huo utawezesha kuimarika kwa upatikanaji umeme katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa pamoja na kuiwezesha kufanya biashara ya umeme katika nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakati alipotembelea eneo litakapojengwa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha Tunduma wilayani Momba, mkoani Songwe.

Inaelezwa kuwa kituo hicho ni moja kati ya vituo vitano vya kupoza umeme vitakavyojengwa kwenye mradi huo.

“Tuna matumaini mradi utakamilika ndani ya miaka miwili kwani umetengwa katika vipande nane, hivyo kutakuwa na wakandarasi wengi watakofanya kazi kwa mpigo, na hii itawezesha kujengwa kwa vituo vitano vya kupoza umeme pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa hadi Rukwa na kipande cha kwenda mpaka wa Zambia,” amesema.

Send this to a friend