Rais Biden athibitisha kuuawa kiongozi wa kundi la Al Qaeda

0
16

Rais wa Marekani, Joe Biden amethibitisha kuuawa kwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda, Ayman al-Zawahiri, katika operesheni ya maafisa wake wa kijasusi.

Akilihutubia taifa kutoka Ikulu mjini Washington DC Agosti 1, 2022, amesema operesheni ya kumtafuta al-Zawahiri imefanyika kwa muda mrefu, na pia aliidhinisha kuuawa kwake wiki iliyopita.

Amesema mshukiwa huyo wa ugaidi alikuwa amejificha pamoja na familia yake katika nyumba moja mjini Kabul, Afghanistan, ambako aliuawa na maafisa wa Marekani.

“Haki imetendeka. Kama wewe ni tishio kwa watu wetu, Marekani itakupata. Haijalishi itachukua muda gani, lakini tutakupata,” amesema.

Al Zawairi, ambaye aliuawa siku ya Jumapili, alikuwa naibu wa mwanzilishi wa kundi la Al Qaeda, Osama bin Laden, na inaaminika kuwa alichukua uongozi wa kundi hilo baada ya kifo cha Bin Laden mwaka wa 2011, pia ni mmoja wa watu walioshutumiwa kupanga mashambulizi ya kigaidi Marekani mwaka 2001.

Taarifa hiyo ilitolewa muda mfupi baada ya viongozi wa Taliban mjini Kabul kusema kwamba shambulizi la Jumapili kwenye makazi binafsi mjini humo lilifanywa kwa kutumia drone ya Marekani huku Msemaji wa serikali ya Taliban ya Afghanistan, Zibihullah Mujahid kupitia taarifa yake akikemea vikali shambulizi hilo na kusema ni kinyume na sheria za kimataifa inayokiuka makubaliano ya Doha pia.