Rais Samia: Serikali yangu imejielekeza kutatua kero za wananchi

0
17

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya awamu ya sita haina mpango wa kukata maeneo kwa kuyapandisha hadhi, badala yake inajielekeza katika kutatua shida za wananchi zilizopo nchini.

Ameyasema hayo leo Agosti 5, 2022 akiwa Mbalizi mkoani Mbeya baada ya kupokea ombi kutoka kwa mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza la kutaka Mbalizi kupandishwa hadhi na kuwa halmashauri ya mji ili iwasaidie wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.

Rais Samia awaonya viongozi matumizi mabaya ya fedha za Serikali

Rais Samia amesema alipokea ombi hilo kutoka kwa viongozi, na kuwaeleza wananchi hao kwamba Serikali yake imejielekeza kwenye vipaumbele ikiwemo utatuzi wa shida za wananchi.

“Kwa sasa hivi, wananchi wangu wa Tanzania wana shida chungu nzima, wanataka umeme, wanataka madarasa. Mwaka jana tulijenga madarasa 15,000 ya sekondari,” amesema.

Ameongeza “Wananchi mnataka vituo vya afya, mnataka maji. Tukisema tunakatana halmashauri, na Tanzania nzima inataka kukatwa maeneo, hatutaweza, uchumi wetu bado haujaruhusu. Acha tumalize shida za wananchi, tukishamaliza tutakwenda kukatana kwenye maeneo.

Mbali na hayo Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ambalo litamruhusu mama mjazito kuingia na mume wake wakati wa kujifungua.

“Hospitali hii kwenye vile vyumba vya kujifungulia tumeweka na mwenza wako atakuwepo humo ndani, kwa sababu kazi ya kutengeneza kiumbe mliifanya pamoja akushuhudie siku unayotoa kiumbe kile na aone hali unayokuwa nayo siku ile ili wajenge mapenzi upande wetu” amesema.

Send this to a friend