Askofu Kilaini: Kutumika jeneza Simba Day ni dhihaka kwa dini na imani

0
19

Baada ya Mwanamuziki Tunda Man kuingizwa akiwa ndani ya jeneza kwenye tamasha la ‘Simba Day’ Agosti 8, 2022 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, baadhi ya viongozi wa dini wamesema kitendo hicho ni dhihaka dhidi ya dini ya Kikristo na kinapaswa kulaaniwa.

Askofu wa Msaidizi wa Kanisa la Katoliki Jimbo la Bukoba, Dk Methodius Kilaini amesema kitendo hicho ni kibaya na kinapaswa kukemewa kwa kuwa kinadhalilisha dini pamoja imani za watu wengine hivyo atawasiliana na viongozi wenzake kuona namna gani watalikemea ili lisitokee tena.

“Hiki ni kitendo kibaya ambacho kinadhalilisha dini na imani za watu. Hakipaswi kuendelea kuwapo kwa mara nyingine hata kama ni masuala ya michezo,” amesema Askofu Kilaini.

Naye Askofu wa Tanzania Assemblies of God (TAG), Jimbo la Kigoma, Mulenda Kalama amesema kitendo cha kubeba jeneza na kuweka msalaba juu kinaashiria maafa katika siku zijazo katika maeneo hayo ya mpira.