Kenya: Mgombea awatupia lawama wananchi kwa kumnyima kura baada ya kula hela zake

0
33

Mgombea aliyekuwa Mwakilishi katika Baraza la Kaunti (MCA) ya Meru, Festus Kithinji  ambaye kura alizopata hazikutosha kumpa ushindi amegeuka gumzo baada ya kuchapisha video inayomuonesha akisikitika jinsi alivyomaliza akiba yake yote wakati wa uchaguzi.

Mgombea huyo alikuwa akigombea kiti cha uwakilishi wa Kata ya Mbeu kwa tiketi ya Wiper, amesema amehisi kukata tamaa baada ya kuwekeza mtaji na muda mwingi katika kampeni zake, lakini akashindwa kwa kura nyingi.

“Nilivyosimama hapa salio la akaunti yangu ya benki linasomeka sifuri, niliweka juhudi zote na sasa mnanipa hivi, nyie watu ni waongo kwanini mlinidanganya, kuniita mheshimiwa na hamjanipa kura zenu. Hiyo si haki, hata Mungu atawahukumu ninyi watu,” amesema huku akizuia machozi.

Ameongeza kuwa “Watu watakuja na pesa (2027). Siwezi kuahidi kuwa nitakuwa na pesa za kutosha kwa ajili yenu. Kwa kweli najisikia kukata tamaa na kuumia moyo.  Ninahisi kama niache siasa, inasikitisha sana.”

Katika video yake ya  pili ambayo ameitoa saa chache baada ya ile ya kwanza, Kithinji amesisitiza kwamba azimio lake la kisiasa bado halijayumba na itakapofika mwaka 2027 jina lake litapigiwa kura tena.

Licha ya malalamiko hayo, Kithinji amemtakia kila la heri  Mwakilishi Mteule wa Mbeu.

Send this to a friend