William Ruto alizaliwa Desemba 21, 1966 katika kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya, na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi ya Kamagut, kisha akajiunga na Sekondari ya Wareng iliyoko Eldoret.
Baada ya kumaliza elimu ya Sekondari, alijiunga na Shule ya Kapsabet iliyoko Nandi ili kuendelea na elimu yake, na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi na kupata shahada ya kwanza katika masomo ya Zoolojia na Botania.
Mwaka 1990 alipata udhamini wa masomo ya shahada ya uzamili katika chuo hicho.
Mnamo 1992, alijiunga na Chama cha Kenya African National Union (KANU), katika kampeni ya uchaguzi ili kumuunga mkono mgombea urais na mwanzilishi wa chama hicho, Daniel Arap Moi.
Baadaye aliteuliwa kuwa Mbunge wa bunge la Eldoret Kaskazini mwaka 1997, kisha 2002 alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, na mwaka huo huo alichaguliwa tena kuwa Mbunge.
Alitangaza kuwania Urais wa mwaka 2006, uamuzi ambao haukuungwa mkono na wenzake wa KANU, hivyo aliwasilisha jina lake kwenye Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) lakini hakupata uteuzi.
Ruto: Sitokuwa na kisasi na mtu yeyote
Ruto aliachana na KANU na kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo 2008 na Waziri wa Elimu 2010, kisha akajiuzulu uwaziri na kuendelea kuwa mbunge 2011.
Amewahi kushtakiwa katika kesi mbalimbali za jinai katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Chama cha ‘Law Society of Kenya’ (KSK) kiliwaorodhesha watu waliodaiwa kuwa mafisadi akiwemo William Ruto na kuwaomba wananchi kutowapigia kura, lakini alishinda ubunge katika uchaguzi uliofuata.
Mwaka 2009 alidaiwa kuuza mahindi kinyume cha sheria ambayo ni mali ya Serikali, hata hivyo madai hayo yote yalibatilishwa na Naibu spika wa Bunge.
Ruto aliwahi kuajiriwa kama mwalimu katika shule mbalimbali za Sekondari za Sirgoi na Kamagut kabla ya kuingia katika siasa.
William Ruto ana watoto sita aliowapata na Bi. Rachel Chebet ambao wameoana tangu mwaka 1991.