Waziri Nape Nnauye amesema Serikali inaangalia namna itakayosaidia kupunguza gharama za bando.
Uwekwaji wa mkongo wa taifa umeipa thamani mlima Kilimanjaro na kuongeza usalama zaidi kwa watalii.
Kutokana na malalamiko ya Watanzania kuhusu kupanda kwa gharama za huduma ya intaneti nchini Waziri wa Habari, Mawasilaiano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali iko katika mchakato wa kuangalia namna ya kupunguza gharama za uzalishaji utakaosaidia kupungua kwa bei ya bando.
Akizungumza mapema leo katika mahojiano na kipindi cha Power Breakfast alipokuwa akifafanua kuhusu gharama za intaneti, Waziri Nape amesema ulinganifu wa gharama hizo hufanywa na mashirika ya kimataifa na siyo Serikali kama wengi wanavyodhani.
“Ulinganifu huu wa gharama za usafirishaji wa data haufanywi na Serikali, unafanywa na mashirika makubwa ya kimataifa duniani na umefanywa kwa nchi zote siyo Tanzania peke yake,” amesema.
Nchi 10 Afrika zenye gharama kubwa zaidi za intaneti
Aidha, amegusia kuhusu mkongo wa Taifa katika mlima Kilimanjaro akieleza kuwa umeongeza thamani ya mlima huo zaidi pamoja na usalama kwa watalii, kwa kuwa sasa watalii wanaweza kuwasiliana na watu walioko chini na kupata msaada wa aina yoyote wanapokuwa kileleni.
“Katika milima ambayo ina usalama mzuri, mlima Kilimanjaro umeingia katika rekodi,” ameongeza.