Karani wa Sensa Kata ya Majimoto, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi, Kenan Kasekwa, amevamiwa usiku wa kuamkia leo na kuporwa kishikwambi cha kutunzia kumbukumbu za sensa.
Akithibitisha tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Catherine Mashala, amesema karani huyo ambaye ni mwalimu, alivamiwa na mtu aliyevunja kitasa na kuingia chumbani, kisha kubeba kifaa hicho, fedha kiasi cha Sh 760,000, redio na vitu vingine.
“Inavyoonekana alipuliza dawa ya kuwalaza usingizi yeye na familia yake, yule mwizi aliingia chumbani akabeba ka lasketi, kishikwambi, fedha alizozikuta, simu na redio, “alisema Mashala.
Wakati huo huo, Karani wa Sensa ya Watu na makazi Jiji la Arusha, Sarapia Kiwango, ameporwa kishikwambi chake, wakati akijiandaa kwenda kuhesabu makundi maalum, usiku wa kuamkia leo, huku mumewe akijeruhiwa.
Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi katika Jiji la Arusha, Maneno Maziku, amesema, karani Kiwango aliporwa kishikwambi hicho na kwamba alipatiwa kingine kuendelea na kazi.
“Ni kweli aliporwa kishikwambi, huku mume wake akijeruhiwa kichwani, lakini ameshapewa kishikwambi kingine anaendelea na kazi, pia majeruhi hali yake inaendelea vizuri,” amesema.
Chanzo: Habarileo