Rais wa Marekani, Joe Biden amesema Serikali ya Marekani itasamehe kiasi cha dola 10,000 [sawa na TZS milioni 23.3] ya mikopo kwa kila mwanafunzi kwa mamilioni ya wanafunzi wa zamani wa vyuo vikuu walio na madeni nchini humo.
Ameyasema hayo Jumatano Agosti 24, 2022 ikiwa ni ahadi yake aliyoiweka katika kampeni ya mwaka 2020 endapo ataingia katika Ikulu ya White House.
Pia, Rais Biden atasamehe $20,000 [sawa na TZS milioni 46.6] ya deni kwa wanafunzi wenye uhitaji mkubwa wa fedha nchini humo.
“Kwa kuzingatia ahadi yangu ya kampeni, utawala wangu unatangaza mpango wa kuzipa familia zinazofanya kazi na watu wa tabaka la kati ahueni juu ya malipo ya mkopo wa wanafunzi wa shirikisho mnamo Januari 2023,” aliandika katika mtandao wa twitter.
Hatua hiyo inaweza kuongeza uungwaji mkono kwa wanachama wenzake wa Democratic katika uchaguzi wa bunge la Novemba, lakini baadhi ya wanauchumi wamesema, kitendo hicho huenda kikachochea mfumuko wa bei na baadhi kuhoji iwapo Rais ana mamlaka ya kisheria ya kufuta deni hilo.
Inakadiriwa kuwa Wamarekani milioni 43 wanadaiwa jumla ya $1.6tn [sawa na TZS quadrilioni 3.73] katika deni la shirikisho la wanafunzi.