Shirika lisilo la Kiserikali la TWAWEZA East Africa limezindua ripoti ya matokeo ya utafiti mpya wa Sauti za Wananchi ulioangazia maoni na uzoefu wa Watanzania kuhusu hali ya taifa kati ya Oktoba 2021 na Julai 2022 ikiwa umejumuisha maoni na uzoefu wa wananchi kuhusu tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa wananchi walio wengi, takribani asilimia 64 wameridhishwa na matumizi ya mapato yatokanayo na miamala ya fedha kwa njia ya simu. Katika matokeo ya takwimu yaliyotolewa ni asilimia 24 pekee ya Watanzania ambao wameeleza kuwa hawaridhiki na matumizi ya mapato yatokanayo na tozo za miamala huku asilimia 12 wakieleza kuwa hawana maoni.
Matokeo ya tafiti katika ripoti hiyo yameonesha utayari mkubwa wa watanzania kulipa kodi kwa hiari kwani tafiti zimeonesha kuwa karibu wananchi wote (asilimia 90) wanakubaliana na wazo la msingi kwamba kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi huku takwimu hizo zikifafanua kuwa karibu wananchi wote (takribani asilimia 88) wanasema wangependa kulipa kodi bila shuruti, na wengine (asilimia 67) wanasema si vyema kuficha kipato ili kulipa kodi chini ya kipato, na asilimia 63 ya wananchi wanasema ni wajibu wa wote kulipa kodi.
Vilevile, wananchi wameonesha dalili kwamba wangeunga mkono zaidi tozo hizo iwapo wangekuwa na taarifa kamili za namna mapato yanayopatikana yanavyotumika, ambapo takribani asilimia 63 wanasema wangekuwa tayari zaidi kulipa ushuru kama wangefuatilia jinsi fedha zinavyotumika, huku asilimia 39 wakisema wanajua jinsi fedha hizo zinavyotumika, na asilimia 44 wakieleza kuwa wanaweza kujua kwa urahisi kutoka serikalini matumizi ya fedha zilizokusanywa.
Kwa upande mwingine tafiti hiyo inaonesha kuwa wananchi walio wengi (asilimia 67) wanakubali kwamba tozo ni njia muhimu ya serikali kupata mapato na kwamba inahakikisha kuwa kila mtu anachangia maendeleo ya taifa, huku asilimia 66 ya Wananchi walikubaliana na pendekezo kwamba tozo yenyewe siyo tatizo bali gharama za miamala zinazotozwa na watoa huduma.