Rais Samia Suluhu Hassan amesema upungufu wa mafunzo kwa askari wa Jeshi la Polisi unachangia mmomonyoko wa maadili katika baadhi ya maeneo ndani ya Jeshi la Polisi.
Amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi Mkoani Kilimanjaro, ambapo amesema askari wasio na sifa ndio wanaolipa fedheha Jeshi la Polisi, hivyo Serikali imetoa bilioni 11 ili askari wapate mafunzo.
Aidha, amesema Serikali itahakikisha Jeshi la Polisi linaingia haraka kwenye mfumo wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuweza kuendana na kupambana na mbinu za wahalifu.
“Dunia inaendelea kubadilika tena kwa kasi kubwa katika matumizi ya teknolojia, kwa hiyo na sisi kama sehemu ya dunia hatuwezi kupitwa na mabadiliko haya, hasa ikizingatiwa kuwa wahalifu nao huwa wanabadilisha mbinu zao jinsi teknolojia inavyokua,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo Rais Samia amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Ramadhan Kingai kuhakikisha unafanyika upelelezi na kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kumuweka mtuhumiwa mahabusu.