Rais Samia Suluhu Hassan amesema suala la ubaguzi wa kijinsia katika biashara linahitaji kuzungumziwa katika ngazi ya Umoja wa Afrika ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuziba pengo hilo.
Amesema hayo leo Septemba 12, 2022 wakati akishiriki Kongamano la Wanawake na Vijana wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) katika ukumbi wa JNICC, Jijini Dar es Salaam.
“Nawashukuru wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kwa kufanya maamuzi ya busara ya kuanzisha itifaki maalum ya wanawake na vijana, kwa lengo la kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye biashara,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa changamoto za mitaji zinazowarudisha nyuma wanawake na vijana katika biashara, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kurekebisha mifumo ya kodi na tozo pamoja na kuyataka mabenki kufungua madirisha maalumu kwa ajili ya kuwakopesha wanawake na vijana kwa riba nafuu.
Mbali na hayo, Rais Samia amesema ni jukumu la watu wote kuhakikisha mabadiliko ya kiuchumi yanafanikiwa katika bara la Afrika ili kuleta maisha bora.