Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu itakayofanyia kazi tozo zenye utata kwenye miamala ya fedha za kielektroniki.
Ameyasema alipokuwa katika mkutano wa hadhara Sirari, Wilaya ya Tarime mkoani Mara na kubainisha kuwa Serikali itaendelea kutoza tozo za uhawilishaji fedha za kielektroniki na kodi nyinginezo, huku akibainisha kuwa baadhi ya mabadiliko yatafanyika ili kuakisi mapendekezo ya chama tawala kuhusu suala hilo.
“Kufuatia mapendekezo ya chama [CCM], Serikali imeunda timu ya wataalamu ambayo tayari imeanza kufanya uchambuzi wa kina wa suala hilo,” amesema na kuwataka Watanzania kuwa na subira.
Rais Samia: Kuna pengo la ubaguzi wa kijinsia kwenye biashara
Aidha, Nchemba amesema wataalam wanaangalia njia bora na rafiki zaidi ya kukusanya mapato kwa namna ambayo itazingatia maslahi ya Watanzania.
“Tumepokea mapendekezo kutoka kwa chama tawala. Inawezekana kwamba katika mchakato [wa kufanyia kazi tozo], tunaweza kuwa tumedhulumiana, jambo ambalo ni la kawaida kwa wanadamu. Niruhusu, hata hivyo, niseme kwamba nchi haiwezi kuendelea bila mapato,” ameongeza.
Wakati baadhi ya wananchi wakiendelea kulalamika kuhusu tozo hizo, utafiti uliofanywa hivi karibuni na Twaweza ulionesha kuwa asilimia 64 ya Watanzania wanaridhishwa na matumizi ya tozo hizo.