Makala aliyoandika Rais Samia Suluhu leo Dunia ikiadhimisha Siku ya Demokrasia

0
17

Na Rais Samia Suluhu Hassan

Mwaka 2007, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulifanya uamuzi wa kuzitaka nchi duniani kuadhimisha siku ya Demokrasia kila ifikapo tarehe 15 Septemba, ya kila mwaka.

Siku hii inaadhimishwa kwa madhumuni ya kukuza na kuendeleza demokrasia katika kila nchi kwa mifumo inayokubalika. Hivyo, katika siku ya leo, sisi kwa upande wetu kama Nchi tunapaswa kuzungumzia yanayoikabili demokrasia yetu.

Katika kuadhimisha siku hii, hakuna budi, ila kuwashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kudumisha Amani na utulivu nchini. Hapa, niungane na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake alioutoa leo kwa dunia kwamba; Nanukuu

“Sasa ni Wakati wa kuhakikisha kwamba Demokrasia, Maendeleo na Haki za Binadamu ni mambo yanayoshikamana”.

“Sasa ni wakati wa kusimama na misingi ya kidemokrasia, ya Usawa, Ushirikiano na Umoja”

Pamoja na kwamba kwa mwaka huu 2022, Umoja wa Mataifa umejielekeza kuzungumzia demokrasia kwa vyombo vya habari, na kwa kuwa hakuna mfumo mmoja wa kuendesha demokrasia duniani, kwa upande wetu, tunajielekeza kuzungumzia jambo ambalo limekuwa likidaiwa sana na Vyama vya Siasa hapa nchini.

Vyama vya Siasa vimekuwa vikidai kuruhusiwa kuendelea kufanya kazi za kisiasa, hususan, kufanya mikutano ya hadhara na wanachama wao. Serikali itumie fursa hii kueleza kwamba, Kikosi Kazi kinachoratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kimeendelea kusisitiza kutolewa kwa ruhusa ya kuendesha mikutano ya vyama vya Siasa, ila wameonesha wasiwasi kwenye sheria na kanuni zinazosimamia suala hilo.

Demokrasia ni mchakato unaohusu namna ya uendeshaji wa mambo kuendana na matakwa ya Wananchi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kwa kufuata Mila na Desturi za nchi husika, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi. Tanzania tupo katika hatua mbalimbali za kutanua wigo wa ushirikishwaji wananchi kwa kuzingatia mazingira yetu, huku tukiongozwa na moyo wa maridhiano yanayotujengea usawa, mshikamano na umoja.

Hivyo basi, kwa muktadha huu, nashauri kwamba tusubiri maoni na mapendekezo ya Kikosi Kazi juu ya marekebisho ya Sheria na Kanuni hizo, na kwamba suala hili litatolewa tamko siku chache zijazo.

Kazi Iendelee!

Send this to a friend