Wateja wa M-Pesa na mapato ya Vodacom vyapungua
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom imesema kutokana na kuanzishwa kwa tozo za miamala ya kielekroniki imepelekea kushuka kwa mapato ya kampuni hiyo ikiwemo kupungua kwa wateja wa M-Pesa.
Amesema hayo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo Jijini Dar es Salaam wakati akieleza athari za tozo kwa mapato ya kampuni hiyo.
“Kampuni iliripoti mapato ya huduma ya shilingi bilioni 956.5 ambayo yameshuka kwa asilimia 1.0 ikilinganishwa na mapato ya mwaka uliopita. Kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na upotevu wa mapato ya shilingi bilioni 103.8 yaliyotokana na tozo kwenye miamala ya simu kuanzia Julai 2021,” amesema Mihayo.
Ameongeza kuwa mapato ya M-Pesa ni shilingi bilioni 329.5, yakiwa yamepungua kwa asilimia 7.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 356.8 iliyopatikana katika mwaka wa fedha uliopita.
Kampuni hiyo imesema jambo la kutia moyo ni mapato ya data ya simu (intaneti) ambayo yameongezeka kwa asilimia 18.9 na kufikia shilingi bilioni 204.0.
Aidha, ameongeza kuwa kitendo cha Serikali kupunguza tozo kimeleta ahueni na kurejesha ari ya upatikanaji wa mapato.