Kutokana na Watanzania wengi kushindwa kumudu gharama za matibabu, Serikali imetoa pendekezo la kuruhusu suala la bima ya afya kuwa la lazima kwa Watanzania wote ili kuwawezesha wananchi kuchangiana gharama za matibabu.
Akizunguma na vyombo vya habari leo Septemba 27, 2022 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameeleza kuwa Serikali tayari imekamilisha rasimu ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya na imewasilisha rasimu ambayo imesomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Bunge la Tanzania.
Msako wanaowatumia walemavu kujipatia pesa
Kupitia Sheria hiyo amefafanua kuwa, anayeumwa na kuhitaji matibabu atachangiwa gharama za matibabu na wale ambao watakuwa hawaumwi kwa kipindi husika. Hivyo, utaratibu huo utaondoa hali iliyopo sasa inayomlazimu mtu kubeba mzigo peke yake wa kulipa gharama kubwa za matibabu anapokuwa ameugua.
“Kupitia utaratibu huu, ni kawaida kwa mwananchi kulipa kiwango kidogo cha fedha kwa kujiunga na bima ya afya na akapatiwa matibabu ya gharama kubwa kuliko kiasi cha fedha alicholipia wakati anajiunga na bima ya afya.
Pili, utaratibu huu unampa mtu uhuru wa kutafuta fedha na kulipia kadi ya bima ya afya bila ya kuwepo hali ya dharura kama ile ambayo mtu huwa nayo wakati anapohitaji kulipia papo kwa papo huduma za matibabu,” amesema.
Aidha, Waziri Ummy amebainisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayekamatwa, kufungwa au kulipishwa faini kwa kushindwa kulipia bima ya afya isipokuwa Serikali inatarajia kufungamanisha umiliki wa kadi ya bima ya afya na upatikanaji wa baadhi ya huduma za kijamii kama ambavyo baadhi ya huduma zilivyofungamanishwa na umiliki wa namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
“Lengo la kufungamanisha umiliki wa kadi ya bima ya afya na baadhi ya huduma ni kuepuka adhabu za kukamata na kushitakiwa mahakamani kwa watu wasio na kadi ya bima ya afya kwa kuwa kufanya hivyo hakutaiwezesha Serikali kufikia lengo la kila mwananchi kupata huduma za afya.” amefafanua.