Uwekaji kope, lenzi machoni chanzo cha upofu

0
27

 

Daktari Bingwa wa Maradhi ya Macho kutoka Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Ahmed Muumin amewashauri wanawake hasa wasichana kuacha kuingiza vitu katika macho yao ikiwemo viini (lenzi) vya urembo ambavyo vitawasababishia kupata upofu wa maisha.

Daktari amesema wapo baadhi ya watu wanaovaa lenzi wanapokwenda kwenye shughuli mbalimbali na mara wanaporudi nyumbani huwa wanasahau kuziondoa na kulala nazo, jambo ambalo ni hatari kwa macho yao.

“Wanapoitoa vidole vyao vikiwa na kucha ukijichuna kioo cha mbele cha jicho au kama umeitoa na kuiweka sehemu ambayo si salama ikaingia vumbi au mchanga na kuitia tena basi anaweza kujisababishia madhara katika jicho,” amesema.

Ameeleza kwamba wengine hupata vidonda baada ya kujichuna katika kioo cha jicho, jambo ambalo linaweza kuleta ulemavu wa uoni.

Aidha, amebainisha madhara ya muda fupi ya uwekaji kope ni kuvimba jicho, kuwasha, kutoka machozi na kusababisha tongo za muda mrefu.

“Unatia kope kwa kutumia gundi ambayo ni kemikali na inapogusana na kioo chako cheupe cha jicho basi unatengeneza hatari kubwa ikiwemo kulika kwa kona ya jicho na kupata ulemavu wa maisha,”ametahadharisha.

Send this to a friend