Baba Mtakatifu Papa Francis amtunuku Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., kutoka Tanzania Nishani ya Msalaba wa Kanisa na Papa kutokana na huduma ya mawasiliano ya kanisa kupitia Radio Vatican Idhaa ya Kiswahili.
Padre Mjigwa anayehudumu katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican amekuwa Mtanzania wa pili kutunukiwa nishani hiyo baada ya miaka sita tangu Mtanzania wa kwanza aliyehudumu katika Baraza hilo, Mama Thabita Janeth Mhella kutunukiwa Nishani hiyo mwezi Septemba 2016.
Padre Mjigwa ambaye ni mwanashirika wa Shirika la Damu Azizi, alikabidhiwa nishani hiyo na Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano la Kipapa, Dkt. Andrea Tornielli kwa niaba ya Papa Francis kufuatia juhudi zake za kuhudumia jamii katika kueneza sauti na miongozo ya Papa katika lugha ya Kiswahili kupitia Radio Vatican kwenye mataifa yanayozungumza lugha hiyo.
Utangazaji katika lugha ya Kiswahili kwenye Radio Vatican ulianza mapema mwezi Novemba 1961 baada ya Wamisionari wa Afrika (White Fathers) kuanza kuandaa makala kwa lugha ya Kiswahili kufuatia uzinduzi uliofanywa na Papa Mtakatifu Yohane XXIII na kupelekea kurushwa matangazo hayo ya kila siku kwa Afrika.