Muuguzi afikishwa mahakamani kwa kumlawiti mgonjwa

0
19

Joseph Kiungi (25) muuguzi wa Zahanati ya Saint Theresia wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumlawiti binti wa kidato cha pili alipokwenda kupatiwa matibabu.

Akisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, James Mhanus Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mazoya Luchagula amesema Kiungi alitenda kosa hilo Oktoba 13 na kwamba upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo kuiomba mahakama isome maelezo ya kosa ili ianze kusikilizwa.

Akitoa ushahidi binti anayedai kufanyiwa ukatili huo ameieleza mahakama kuwa alikwenda kwenye Zahanati hiyo kuchoma sindano ya tetenasi na kupokelewa na muuguzi huyo aliyemwelekeza kwenda chumba cha sindano.

Ameongeza kuwa walipofika chumba hicho muuguzi alimwambia avue nguo za ndani kisha ainame kwa kuwa kuna kidonge anatakiwa kumwekea sehemu ya haja kubwa kabla ya kumchoma sindano, ndipo binti huyo akatekeleza maagizo aliyopewa.

Akiendelea kutoa ushahidi huo amesema baada ya kuinama alihisi maumivu makali ndipo alipogeuka na kumwona mshtakiwa akiwa anatekeleza kitendo hicho, hivyo akapiga yowe na kukimbia kutoka chumba hicho hadi eneo la mapokezi na kuomba simu ili awapigie wazazi wake kuwaeleza kitendo hicho.

Ameiambia mahakama kuwa baada ya baba yake kufika hospitalini hapo walipiga simu Polisi na kumkamata mtuhumiwa, na baada ya taratibu kufuatwa binti alifikishwa hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya vipimo ili kuthibitisha kitendo hicho.

Mshtakiwa amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo yalimtaka kuleta wadhamini wawili watakaosaini hati ya shilingi milioni 10 kila mmoja pamoja na mshtakiwa mwenyewe.

Send this to a friend