Zuchu adaiwa kuiba sehemu ya wimbo wa injili, milioni 500 hatarini kumtoka

0
29

Msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Zuhuru Othman maarufu Zuchu huenda akalazimika kulipa kiasi cha TZS milioni 500 baada ya kudaiwa kuiba kipande cha wimbo wa msanii wa Injili, Enock Jonas na kukiweka katika wimbo wake.

Katika malalamiko hayo Jonas, amedai Zuchu amechukua sehemu ya kibwagizo na staili ya kucheza katika wimbo wake wa ‘Wema wa Mungu’ ambao ulitoka mwaka 2012 na kujulikana zaidi kwa jina la ‘Zunguka’ kisha kuutumia katika wimbo wake mpya ‘Kwikwi’.

BASATA yampa Harmonize siku mbili

Kwa mujibu wa Mwananchi, Enock amedai amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya mazungumzo na upande wa Zuchu kushindikana kwa kumwambia kuwa katika madai hayo kuwa hawawezi kumlipa.

kupitia barua iliyoandikwa na kampuni ya wanasheria ya Gerpat Solution, mmoja wa wanasheria hao Gerlad Magubuka amesema tayari wameshawapelekea wahusika barua ya madai hayo na nakala nyingine wamepeleka Taasisi ya Hakimiliki Nchini (Cosota) na Shirikisho la Wanamuzi Tanzania (Shimuta).

Kwa upande wao Cosota kupitia Katibu Mtendaji wake, Doreen Sinare, amekiri suala hilo kutua mezani kwake na kueleza kilichofanyika ni wasanii wenyewe kuandikiana barua na wao wamepelekewa kama taarifa hivyo hawawezi kusema lolote kwa sasa wameacha wasanii wenyewe ndio wawasiliane kwanza na baadaye wao watakuja kuichambua na kuitolea tamko.

Chanzo: Mwananchi.

Send this to a friend