Timu yaundwa kuchunguza vifo vya watu wawili waliouawa na Polisi Morogoro
Jeshi la Polisi limeunda timu maalum ili kuchunguza mauaji ya watu wawili na wengine wawili kujeruhiwa katika kijiji cha Ikwambi, Kata ya Mofu, Tarafa ya Mgeta wilayani Kilombero mkoani Morogoro kwa madai ya viashiria vya uvunjifu wa amani vilivyoonekana baada ya wananchi jamii ya wakulima kulalamikia kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo katika mazao na wenzao wawili kushambuliwa Oktoba 22, 2022
Akitolea ufafanuzi juu ya tukio hilo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura amesema timu hiyo ambayo imeundwa chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na taasisi nyingine za Serikali ni kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi huru utakaowezesha kupata majibu ya chanzo cha tukio hilo na kubaini uwiano wa matumizi ya nguvu iliyotumiwa na Jeshi la Polisi kudhibiti vurugu hizo.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea IGP Wambura amewataka wananchi wa kijiji hicho kuwa watulivu pamoja na Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero kutoa ushirikiano wakati timu hiyo inapokwenda kufanya kazi hiyo ya uchunguzi.
Wananchi wachoma moto ofisi ya Kijiji na kusababisha vifo vya watu wawili
Aidha, amewaagiza askari wote waliohusika kwenye tukio hilo wakae kando kupisha uchunguzi ili timu hiyo iwe na nafasi nzuri ya kuweza kutimiza wajibu wake wa kuweza kuja na majibu na matokeo sahihi ya uchunguzi, ili Watanzania waweze kufahamu ukweli wa tukio hilo.
Katika taarifa ya Jeshi la Polisi imedai Oktoba 23, 2022 majira ya mchana, Askari Polisi walifika kwenye eneo hilo kwa lengo la kuwaokoa viongozi ambao walidaiwa kukamatwa na jamii ya wakulima na kufungiwa kwenye ofisi ya kijiji, lakini kulitokea tafrani ambazo zilisababisha matumizi ya risasi za moto pamoja na mabomu ya machozi na kupelekea mauaji ya watu hao wawili