Matokeo Sensa: Watu milioni 16.8 waongezeka ndani ya miaka 10

0
18

Rais Samia Suluhu Hassan amesema jumla ya idadi ya Watanzania ni 61,741,120 huku wanawake wakiongoza kwa idadi ya watu 31,687,990 sawa na asilimia 51 huku wanaume wakiwa 30,053,130 sawa na asilimia 49.

Ameyasema hayo leo Oktoba 31, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambapo amesema idadi hiyo ni ongezeko la watu milioni 16.8 sawa na asilimia 3.2 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Miaka kumi iliyopita Tanzania ilikuwa na watu 44, 928, 923 hii inaonyesha kumekuwepo na ongezeko la watu milioni 16,812,197 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 ya waliokuwepo kati ya mwaka 2012 na mwaka 2022,” amesema.

Ameongeza kuwa Mkoa wenye idadi kubwa ya watu Tanzania ni Dar es Salaam wenye idadi ya watu 5,383,728 ukifuatiwa na Mkoa wa Mwanza wenye jumla ya watu 3,699,872, huku jumla ya idadi ya majengo Tanzania ikiwa ni 14,348,372 ambapo kwa Tanzania bara ni 13,907,951 na upande wa Zanzibar ikiwa na idadi ya majengo 440,421.

Send this to a friend