Bodi la Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeufungia uwanja wa Sheikh Amri Abeid wa jijini Arusha kutumika katika michezo ya ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
TPLB imesema eneo la kuchezea (pitch) la uwanja huo halina majani ya kutosha kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya kanuni za leseni za Klabu, hivyo kuufanya uwanja kutokuwa salama kwa watumiaji pamoja na kupunguza ubora wa picha za matangazo ya televisheni.
Kufuatia maamuzi hayo, Bodi ya Ligi imezitaka timu za Polisi Tanzania (ligi kuu ya NBC) na Mbuni FC (Ligi ya Championship) ambazo zilikuwa zikitumia uwanja huo kwa michezo ya nyumbani, kuchagua uwanja mwingine kwaajili ya michezo hiyo.
Aidha, Bodi imesema inaendelea kuzikumbusha Klabu za Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Championship na First League kuendelea kuboresha na kutunza miundombinu ya viwanja vyao vya nyumbani kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo ili michezo ya ligi ichezwe kwenye viwanja bora vinavyosaidia kuongeza ushindani na thamani ya ligi.