Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na mradi wa maji uliozinduliwa Kigamboni, anatumaini mgao wa maji unakwenda kupungua katika jiji la Dar es salaam baada ya mvua kuchelewa kunyesha na kusababisha Mto Ruvu kupungukiwa maji.
Amesema mradi huo pamoja na kuhudumia Wilaya ya Kigamboni lakini pia unalenga kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Saaam.
Hayo yamebainishwa leo aliposhiriki hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Maji, Ugawaji wa Mitambo ya Kuchimbia Visima na Mabwawa pamoja na makabidhiano ya Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda Kisarawe II iliyofanyika Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Rais Samia akemea viongozi kujimilikisha vyama vya siasa
“Taarifa tulizopata ni kwamba mvua zimenza, tumuombe Mungu mvua za kheri ziendelee ili mito yetu ijae na chanzo hiki kibakie kwamba ni akiba, pale ambapo tutapata upungufu basi tunajua tuna akiba ya kutosha Kigamboni na wananchi waweze kupata huduma ya maji,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inatambua kuwa mradi huo wa Kigamboni ni wa kupunguza makali ya ukosefu wa maji lakini suluhisho la uhakika zaidi kwa changamoto hiyo ya maji kwa jiji la Dar es Salaam ni bwawa la Kidunda pindi utakapokamilika.
Hata hivyo ametoa agizo kwa DAWASA kusambaza maji katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam bila kuwepo na upendeleo wa aina yoyote pamoja na kuwasihi wananchi kulinda vyanzo vya maji ili kusiwe na shida ya maji wala shida ya umeme.