Elimu muhimu kuhusu unywaji maziwa na umezaji dawa

0
45

Chanzo kikuu cha mwingiliano wa dawa na maziwa ni madini yaliyomo katika maziwa yajulikanayo kwa jina la kitaalamu kama ‘Calcium.’ Katika mwili, madini haya yanafanya kazi ya kuimarisha mifupa na meno, ufanyaji kazi ya misuli na mfumo wa fahamu.

Unapokunywa maziwa muda mfupi baada ya kumeza dawa, madini haya huchangamana na dawa na kutengeneza kitu ambacho hakiwezi kupenya katika kuta za tumbo na kuingia kwenye damu kwa ajili ya utendaji kazi yake. Hali hii hupelekea kuwa na kiasi kidogo sana cha dawa katika damu hali ambayo inaweza kuleta matokeo hasi mfano, kutokupona (kwa sababu wadudu hawajafa), kuongeza uwezekano wa wadudu kuwa sugu dhidi ya dawa.

Je! Ni dawa zipi zina mwingiliano hasi na maziwa?

Kuna dawa nyingi zenye mwingiliano hasi na maziwa na hivyo ni vyema kumuuliza mfamasia anayekupa dawa hizo ili kujua kama kuna mwingiliano au la.

Baadhi ya dawa zenye mwingiliano na maziwa ni;
•Dawa jamii ya ‘ciprofloxacin’ dawa hii inajulikana sana kutibu homa ya tumbo na ile hali ijulikanayo sana katika jamii kama mkojo mchafu.

•Dawa jamii ya ‘Tetracycline.’ Dawa hii ilijulikana sana kipindi cha nyuma kama rangi mbili.

Unashauriwa kunywa maziwa masaa fatu hadi nne baada au kabla ya kumeza dawa. Pia ikumbukwe kuwa si maziwa tu yanaweza kuleta mwingiliano huo, bali hata bidhaa au chakula kilichoandaliwa na maziwa kama ”yoghurt”  inaweza kuleta matokeo yale yale.

Aina ya vyakula vinavyoimarisha kumbukumbu

Je! Ni dawa zipi zina mwingiliano chanya na maziwa, na kitu gani kinasababisha mwingiliano huo?

Maziwa ni moja ya chanzo kikubwa cha mafuta (fats), baadhi ya dawa huihitaji sana mazingira ya uwepo wa mafuta katika kuta za tumbo ili ziweze kupenya kwa urahisi na kuingia damuni.

Mfano wa dawa hizo ni dawa maarufu sana kwa jina la mseto (Artemether lumefantrine) au ALU inayotumika kutibu ugonjwa wa malaria. Unashauriwa kumeza dawa hizo na maziwa au kunywa maziwa muda mfupi baada ya kumeza dawa jamii hiyo, dawa hizo hazidhuriwi na madini yaliyo katika maziwa.

Hivyo basi, ni vyema kuijua dawa unayomeza ili uweze kufahamu kama inamwingiliano hasi au chanya ikimezwa pamoja na maziwa.

Chanzo: PharmHealthTz

Send this to a friend