Bodi ya Mikopo yafungua dirisha la rufaa kwa ambao hawajaridhishwa na mikopo

0
9

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la rufaa ili kutoa fursa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa hivyo kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema dirisha hilo la rufaa litakuwa wazi kwa siku saba kuanzia Novemba 13 hadi 20 mwaka huu na kwamba rufaa kutoka kwa wanafunzi zinapaswa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao.

“Hadi leo (Novemba 13, 2022), tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali, hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao,” amesema.

Kwa mujibu wa Badru, lengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa.

Send this to a friend