Ripoti kamili ajali ya Precision Air kutolewa baada ya miezi 12

0
15

Kufuatia ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022, leo Kikao cha Baraza la Mawaziri kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan kimekutana jijini Dodoma.

Baraza la Mawaziri limepokea taarifa ya awali juu ya ajali hii na hatua zilizochukuliwa mara baada ya ajali.

Baraza la Mawaziri limewaelekeza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu waliotoka nje ya nchi kufanya uchunguzi wa ajali hii ili kujua chanzo cha ajali na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na ajali na majanga.

Hii ni kwa mujibu wa taratibu na sheria za kimataifa zinazoshughulikia ajali za ndege ambapo Tanzania imesaini makubaliano ya kutekeleza taratibu na sheria hizo.

Aidha, Baraza la Mawaziri limeagiza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe.

Kwa mujibu wa taratibu za kukabiliana na ajali za ndege;

• Timu ya uchunguzi wa ajali na matukio ya ndege inapaswa kutoa taarifa ya awali (Accident Bulletin) ndani ya siku 14.

• Inafuatiwa na ripoti ya awali (Preliminary Report) itakayotolewa ndani ya siku 30

• Na hatimaye ripoti kamili (Final Report) itakayotolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.

Baraza la Mawaziri limewashukuru wote waliohusika katika uokoaji baada ya ajali hii kutokea vikiwemo vyombo vya uokozi, Wananchi wa Bukoba wakiwemo Wavuvi, Wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba, Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera na wengineo.

Pia limewaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi ukifanyika na utakapokamilika watajulishwa matokeo ya uchunguzi huo.

Send this to a friend