Mvua na ukungu vyasababisha ndege ya ATCL kushindwa kutua Bukoba

0
28

Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imeshindwa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera kutokana na hali mbaya ya hewa na badala yake kulazimika kutua katika uwanja wa ndege wa Mwanza.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Ni kweli nimepata taarifa ndege ya Air Tanzania imeshindwa kutua kutokana na hali mbaya ya hewa, kulikuwa na ukungu, mvua, radi na giza uwanja ukawa hauonekani, kwa hiyo rubani akafuta safari na kurudi Mwanza na ametua salama,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Tanzania, Mussa Mbura amesema ndege hiyo imeshindwa kutua kutokana na ukungu na kwamba watu wapuuze uvumi unaoendelea mitandaoni kwamba uwanja wa ndege wa Bukoba umefungwa, kwani uwanja huo unafanya kazi kama kawaida.

Miongoni mwa watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira ambaye baada ya tukio hilo ameandika kupitia mtandao wa twitter na kumpongeza rubani kwa kufanya uamuzi wa kurudi Mwanza, kisha kuiomba Serikali ichukulie kwa uzito suala la uwanja wa ndege mpya wa Bukoba.

Send this to a friend