Kampuni ya RAK GAS huenda ikapoteza 50% ya kitalu cha Pemba Zanzibar

0
17

Na Hamza Bavuai, Unguja

Umebaki mwezi mmoja tu kabla kampuni ya mafuta na gesi kutoka Ras Al Khaima, RAK GAS, ipoteze 50% ya kitalu cha Pemba-Zanzibar.

Hatua hiyo itafikiwa endapo RAK-GAS itashindwa kukidhi matakwa ya mkataba wa mgawanyo wa uzalishaji wa rasilimali ya gesi, uliotiwa saini katika awamu ya saba ya uongozi visiwani Zanzibar, mnamo mwaka 2018 wakati Kamal Ataya akiwa mtendaji mkuu wa kampuni ya RAK GAS.

Haya yaliibuka mwezi Juni katika baraza la wawakilishi wakati Waziri anayehusika na masuala ya mafuta na gesi, Suleiman Masoud Makame, Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi, alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Issa Usi Gavu (Mwakilishi) aliyekuwa Waziri wa Nchi Afisi ya Rais wakati mkataba huo ulipotiwa saini mwaka 2018, juu ya mustakabali ya leseni ya RAK GAS katika kitalu cha Pemba-Zanzibar kutokana na kusuasua kwa uendelezaji wake.

Serikali ya awamu ya nane visiwani Zanzibar, chini ya Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, imeainisha mafuta na gesi kama kipaumbele muhimu katika kupanua wigo wa uchumi wa Zanzibar, hasa hasa baada ya janga la UVIKO-19 kuathiri sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na nia hiyo njema na mazingira wezeshi ya uwekezaji yaliyopo visiwani Zanzibar, iweje mwekezaji pekee katika sekta hii nyeti na yenye matumaini ya kuinua zaidi uchumi wa Zanzibar ashindwe kutimiza matakwa ya mkataba na kupelekea kupoteza 50% ya kitalu ambacho tayari amekwishakifanyia uwekezaji mkubwa katika utafiti wa awali?

Sheria ya Zanzibar ya mafuta na gesi ya mwaka 2016, iliyoandikwa baada ya mafuta na gesi kuondolewa katika mambo ya muungano, imeweka bayana kuwa mwekezaji akishindwa kutimiza programu na kalenda ya shughuli za kiuwekezaji kwa mujibu wa mkataba aliosaini, basi atalazimika kuachia asilimia 50% ya kitalu.

Omar Sharif, katika makala yake ((https://www.ecofinagency.com/public-management/0306-43646-rakgas-may-relinquish-50-of-pemba-zanzibar-block-come-december) kwenye jarida la mtandaoni la Ecofin Agency alitaja mambo yanayoweza kupeleka mwekezaji kushindwa kutimiza masharti ya mkataba, hasa hasa katika kipindi ambacho dunia nzima ilikuwa ikipambana na janga la UVIKO-19 ambalo liliathiri wasafirishaji pamoja na watoa huduma za utafiti katika sekta ya mafuta na gesi.

Sharif alitaja pia mazingira ya kisheria na kisera kuwa kati ya sababu zinazoweza kuathiri uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi.

Aghalabu, wawekezaji wa mwanzo katika sekta hiyo, kama alivyo RAK GAS, hutafuta washirika katika uwekezaji wao ili kuweza kukamilisha mradi kwa wakati. Sharif aliainisha kuwa yawezekana RAK GAS ametafuta mshirika wa uwekezaji bila mafanikio na hivyo kushindwa kuendelea na ratiba ya uwekezaji kwa wakati.

Hata hivyo, si mara ya kwanzs kwa kampuni hiyo kufanya uwekezaji ukanda wa kusini mwa Afrika. Nchini Malawi, kampuni ya RAK GAS ina leseni za vitalu viwili ambazo ilivipata katika utawala wa Rais Joyce Banda. Makala mbalimbali (https://mg.co.za/article/2017-05-15-malawi-oil-contracts-under-probe/,https://www.pwyp.org/pwyp-news/investigate-malawis-oil-contracts/) za majarida ya nchini humo, pamoja na matamko ya viongozi wa serikali ya Malawi katika nyakati tofauti tofauti, yameelezea namna upatikanaji wa vitalu hivyo nchini Malawi ulivyoghubikwa na mazingira yenye utata.

Mathalani, mwaka 2017, baada ya shinikizo kutoka azaki mbalimbali nchini Malawi, taasisi ya kupambana na rushwa nchini humo ilikuwa ikichunguza miamala isiyo ya kawaida inayosemekana kufanywa na kampuni ya RAK GAS mnamo mwaka 2014. RAK GAS iliingia mkataba ya mgawanyo wa uzalishaji na serikali ya Banda siku chache kabla ya uchaguzi wa mwaka 2014.

Malawi ina vitalu sita vya mafuta na gesi katika ziwa Nyasa ambapo RAK GAS ina leseni ya vitalu na. 4 na 5, Pacific Oil Limited ikiwa na kitalu na. 6 na Surestream Petroleum Ltd ya Uingereza ikiwa na vitalu na. 2 na 3.

Mikataba ya mgawanyo wa uzalishaji (PSA) ya vitalu hivi vitatu ilitiliwa saini Mei 12 2014, wakati huo Mtendaji Mkuu wa RAK GAS MB45, Kamal Ataya, kampuni tanzu ya RAK GAS, akiwa pia ndiyo mtendaji mkuu wa kampuni ya Pacific Oil.

Leseni za vitalu na. katika ripoti yake juu ya sekta ya mafuta na gesi nchini Malawi, Oxfam iliainisha kuwa kampuni ya Hamra Oil, mtendaji wake mkuu akiwa Kamal Ataya ilinunua hisa za na kuwa mmiliki mwenye udhibiti katika kampuni ya Surestream Petroleum Ltd (https://mininginmalawi.files.wordpress.com/2017/02/oxfam-2017-malawis-troubled-oil-sector-licenses-contracts-and-their-implications.pdf).

Hii ilipelekea kampuni tatu zenye mtendaji mmoja, kuwa na leseni za vitalu vitano kati ya sita nchini Malawi. Kwa miaka yote – mpaka sasa sekta hiyo nchini Malawi imeghubikwa na hali ya sintofahamu huku chunguzi mbalimbali zikiendelea na azaki zikiishinikiza serikali ya Malawi kuweka wazi mazingira yaliyopelekea umiliki huo wa vitalu. Pia, uendelezaji wa vitalu hivyo umekuwa wakusuasua kwa miaka yote, takriban miaka nane sasa.

Hakuna rekodi zilizowazi zinazoweza kutanabaisha, waziwazi kama mbinu zilizotumika nchini Malawi na Attaya, zilitumika pia Zanzibar na kupelekea RAK GAS kupata leseni za kitalu cha Pemba-Zanzibar. Lakini kutokuwepo rekodi hizi na mazingira yaliyoonekana Malawi kunazaa maswali kadhaa; Je! RAK GAS, chini ya Nishant Dighe imeshindwa kutimiza matakwa ya PSA kutokana na mabadiliko ya uongozi visiwani Zanzibar, i.e. kubadilika kwa mawaziri na watendaji katika sekta ya mafuta na gesi? Je! Ni athari za UVIKO-19 kukosa mshirika wa uwekezaji au kukosa ukwasi wa kuendelea na mradi?

Nakualika katika makala zijazo tuchunguze pamoja namna ambavyo RAK GAS pengine ilijihakikishia ushindi wa kitalu cha Pemba-Zanzibar, kutia saini mkataba wa mgawanyo uzalishaji pamoja na utendaji wake katika utafiti wa mitetemo (2D Seismic).

Ataya alistaafu utendaji katika kampuni ya RAK GAS mwaka 2019 mara tu baada ya utafiti wa awali wa njia ya mitetemo kukamilika katika kitalu cha Pemba-Zanzibar. Rekodi zinaonesha kuwa Nishant Dighe alishika usukani mara baada ya hapo katika kipindi ambacho ratiba ya shughuli za uwekezaji katika kitalu cha Pemba-Zanzibar zimesuasua na kufikia hatua ya kuweza kupoteza 50% ya kitalu ifikapo Desemba.

Mustakabali wa sekta hii visiwani Zanzibar unetegemea sana mazingira yatakayovutia wawekezaji lakini pia uwazi katika majadiliano ya mwekezaji na serikali ya Zanzibar pamoja na mikataba ya mgawanyo wa uzalishaji. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mdhibiti wa sekta ya mafuta na gesi (Zanzibar Petroleum Regulatory Authority – ZPRA), imeweka wazi sheria, kanuni pamoja na mwongozo wa mikataba ya mgawanyo wa uzalishaji (Model PSA) kwa umma kuweza kuisoma japo ni vyema ikatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili pia.

Vipi RAK GAS ikipoteza 50% ya kitalu cha Pemba-Zanzibar? Yawezekana ikawa jambo baya au la kheri kwa sekta hiyo Zanzibar. Baya kwa maana ya kuwa  yaweza ikawatisha wawekezaji wengine wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo Zanzibar, na neema kwa maana ya kuwa inaweza kuwa ni fursa kufungua fursa kwa wawekezaji wengine kwend kuziba pengo pale aliposhindwa RAK GAS.

Kwa vyovyote vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kusonga mbele na suala la mafuta na gesi kama inavyodhihirika katika; 1) Mkataba wa uchakataji wa taarifa za mitetemo na utafutaji wa masoko ya uwekezaji katika sekta uliotiwa saini kati ya serikali na kampuni ya Schlumberger na 2) nia ya kugawa vitalu vingi zaidi katika vitalu namba 9, 10, 11 na 12 mashariki mwa visiwa hivyo ili kuvutia wawekezaji wengi Zaidi.

Ni muhimu kuwa macho ili Zanzibar isijikute katika hali iliyonayo Malawi katika sekta hiyo.

Send this to a friend