Baada ya miaka 12, leo Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa uzalishaji na ugawanaji mapato (PSA) kitalu cha Ruvuma (chenye leseni mbili, Lindi na Mtwara), hivyo kwa mara ya kwanza itapata 75% ya mapato ghafi kutoka kiwango cha awali cha chini ya 68%.
Mkataba wa uzalishaji na ugawanaji mapato katika kitalu hicho ulisainiwa Oktoba 25, 2005 baina ya Serikali, TPDC na Ndovu Resources (Mkandarasi) ambapo Oktoba, 2020, kampuni Ndovu Resource iliuza 50% ya hisa zake kwa kampuni ya ARA Petroleum Ltd na ARA kuwa mwekezaji mkuu katika kitalu hicho.
Akitoa taarifa za mkataba huo, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema mkataba huo ulikuwa na vifungu vinavyosimamia mapato iwapo mafuta yatagunduliwa katika kitalu husika, hivyo kwa kuwa mwekezaji amegundua gesi asilia mkataba wa nyongeza umeandaliwa ili kuongeza vifungu vinavyosimamia mapato ya gesi asilia.
Leo Serikali imetia saini mkataba huo wa nyongeza wa mkataba wa awali wa uzalishaji na ugawanaji mapato baada ya kukamilika kwa majadiliano baina ya timu ya majadiliano ya Serikali na wawekezaji.
“Ndugu zangu wa Lindi na Mtwara, sasa nchi yetu inaanza kuingia kwenye uchumi wa gesi. Sio kwa tukio hili la leo tu, lakini kwa mlolongo wa matukio na jitihada za Serikali. Kule Arusha, tupo kwenye hatua za mwisho za majadiliano kwenye ule mradi wetu wa kuchakata gesi utakao gharimu zaidi ya trilioni 70. Huu utakuwa uwekezaji mkubwa barani Afrika, amesema Makamba.
Ameongeza kuwa mpaka sasa visima viwili vimechorongwa katika kitalu hicho na kugundua gesi asilia kiasi cha futi za ujazo bilioni 466, na tafiti zinazoendelea zinaonesha kitalu hicho kina jumla ya kiasi cha gesi cha futi za ujazo bilioni 1,642.
Faida zitakazopatikana kutokana na mradi ni pamoja na matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme ambayo kwa sasa gesi asili inachangia zaidi ya asilimia sitini (60%) kwenye gridi ya taifa, hivyo utekelezaji wa mradi huu utaongeza kiasi cha umeme unaozalishwa kutokana na gesi asilia, kuendesha viwanda, kutumia majumbani pamoja na kwenye magari.
“Pia eneo la Lindi, serikali imeamua kujenga Chuo (Polytechnic) cha mambo ya mafuta, gesi na umeme, ili kujengea watu wetu uwezo. Lakini pia tutajenga Special Economic Zone [ukanda maalum wa kiuchumi] ndani ya eneo la mradi ili kuchochea maendeleo ya Lindi na Mtwara baada ya mradi kukamilika,” amehitimisha Waziri Makamba.