Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria, Celestine Mushy amefariki katika ajali ya gari mkoani Tanga wakati akielekea Moshi mkoani Kilimanjaro akitokea jijini Dar es Salaam.
Alipata Post-Graduate Diplomasia ya Uchumi kutoka Chuo cha Diplomasia, na Shahada ya Kwanza ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Amewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali Serikalini, na hizi ni miongoni mwao;
Katibu Tawala Msaidizi, Sekretarieti ya Mkoa wa Mtwara (2018-2021).
Balozi na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (2012-2018).
Kaimu Katibu Binafsi wa Waziri Mkuu (2011-2012).
Naibu Katibu Binafsi wa Mawaziri Wakuu wawili na Afisa mkuu wa Utumishi wa Nje, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (2006-2010).
Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Fedha, Ubalozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York (2003-2006).
Afisa Utumishi wa Nje, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (1999-2003).
Kufuatia kifo chake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema amesikitishwa na taarifa ya kifo na kwamba taifa limeondokewa na mwanadiplomasia mahiri na mtumishi makini wa umma.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Balozi Celestine Mushi, Balozi wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu wa nchi yetu katika Mashirika ya Kimataifa, Vienna. Tumeondokewa na mwanadiplomasia mahiri na mtumishi makini wa umma. Mungu amweke mahali pema. Amina,” ameandika Rais Dkt. Samia.
Hayati Balozi Mushy ameacha mke na watoto wawili.