Wakulima wametakiwa kutotumia maziwa kama huduma ya kwanza wanapoathiriwa na viuatilifu wakati wa kuvitumia katika mazao shambani au nyumbani.
Hilo ni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa maziwa yanaipa nguvu sumu hiyo kushambulia seli za mwili wa mwadamu.
Akizungumza mtafiti kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini Tanzania (TPHPA), Dkt. Jones Kapeleka amesema viuatilifu vinapenda kusafiri katika sehemu zenye mafuta kwenye mwili.
Mtafiti ameeleza kuwa “kwa kuwa maziwa yana mafuta, inakauwa rahisi kwa viuatilifu kushambulia seli za mwili kupitia katika mafuta kwenda kwenye damu.”
Aidha, amesema wakulima wanapoathiriwa na sumu hiyo, kitu cha kwanza wanachotakiwa ni kuwekwa kwenye sehemu ya wazi na yenye upepo kisha anywe maji yaliyochanganywa na mkaa uliopondwa wakati utaratibu wa kumpeleka hospitali ikiendelea.
Amesema “kwa watu wanaotumia viuatilifu katika sehemu mbalimbali wanapomaliza kunyunyiza hata kama hawakuathiriwa, wasipendelee kunywa maziwa badala yake wanywe maji kwa sababu ikiwa kuna kiuatilifu kilichojipenyeza mdomoni, maziwa yatahatarisha maisha yake.”